Wanjala, Busaa na Helikopta

Create:
Author: Mwakilishi

Hivi majuzi katika kaunti ya Bungoma, Sale Wanjala alifanya kitendo kilichowashangaza wengi. Kwenye sherehe za kutoa heshima kwa mwendazake Jacob Juma katika uwanja wa Posta, Wanjala alishika chuma ya helikopta ilipopaa. Rubani hakujua ana abiria wa ziada anayeninginia chini ya chombo chake na kufululiza hadi uwanja wa Kanduyi. Kwa safari hiyo ya dakika kumi hivi, maskini alininginia hadi ndege ilipokaribia kutua Kanduyi ndipo akaruka na kupata majeraha. Ilisemekana Wanjala, mfanyikazi wa kibarua, alikuwa amechapa mtindi aina ya busaa alipoyatenda haya.

Nilisomea shule za sekondari katika wilaya ya Bungoma miaka mingi iliyopita. Nilipenda maisha ya watu wa eneo hilo na utamaduni wao. Busaa ilikuwekwo kwa wingi hasa kunakotokeo sherehe ya arusi, tohara, matanga, au sherehe nyingine yoyote. Ukarimu wa jamii hiyo unahakikisha kuwa maskini na tajiri atapata chakula na busaa. Na haikosi ngoma ya isikuti au lipala itapamba moto. Matanga yakiwa ya tajiri au mtu anayesifika, uhondo na kileo kwa wingi pia. Bila shaka hali ilikuwa hivyo katika sherehe ya kumuuaga tajiri Jacob Juma.

Isitoshe, wanasiasa wa mlengo wa upinzani walikuwa wametoa matamshi ya kuwahamasisha wafuasi wao. Walitaka kuhakikisha kifo cha Juma aliyemininiwa risasi na kuuawa Nairobi kimewapa manufaa ya kisiasa. Walidai serikali ilihusika na mauaji hawa na kumtaja makamu wa rais kuwa mshukiwa.

Wanjala hakujua ukweli wa mambo lakini siku hiyo alipata taarifa kutoka kwa jirani yake, Simiyu, kuwa mwanaharakati wa kijijini alikuwa anatoa shillingi mia mbili kusudi watu wafike Kanduyi kuwasikiza vigogo wa chama watakaohutubu kwenye sherehe ya Juma. Wanjala akapata mia mbili zake. Akapitia kwa Mzee Wekesa kuchapa mkebe mmoja wa busaa kabla ya kupanda matatu kuelekea Kanduyi. Waliahidiwa kupata mia nyingine ya kurudi nyumbani baada ya sherehe.

Busaa haijakwisha akasikia mlio wa helikopta ikikaribia uwanja uliokuwa karibu. Kwanza akajificha akifikiria ni ndege ya polisi wanaowasaka wanywaji busaa. Lakini Simiyu akasema ni ndege iliyoleta mwili wa Jacob Juma. Mbio. Wakaifuata na kuona ikitua uwanja wa Posta. Umati ulikuwa unaizingira ndege. Rubani alikifungua kidirisha chake na kuuliza kama huo ni uwanja wa Kanduyi. Akaelezwa sio lakini Kanduyi iko umbali wa dakika chache kutoka hapo.  Ndege ikaanza kupaa na mara Wanjala akazua mpango wa dharura. Lifti hadi Kanduyi na baadaye mia moja. Busaa itakuwa kibao leo. Wanakijiji hawakuamini macho yao Wanjala alipotimua mbio na kuirukia chuma ya helikopta. Huyoo!

Alimka akiwa hospitalini. Wapiga picha, polisi, na mwanawe wa miaka kumi na saba, walikuwa wamekizingira kitanda chake. "Kuna shida gani, junior?" Akamuuliza mwanawe.

- Dkt. Mungai Mutonya | mmutonya@gmail.com. Dkt. Mutonya ni mwalimu na mwandishi wa Kiswahili. Amechapisha Mnada wa Sokomoko, Safari ya Mambosasa, na Mitumba. Soma makala zaidi kwenye blogu yake ya Kiswahili: http://mmutonya.wix.com/blogu.

Comments

Mwakilishi     Mon, 11/23/2009 @ 12:16am

Umaskini! Umaskini! Umaskini! Kukosa matumaini maishani na kukanganywa na viongozi wa kidini na wa kisiasa kunachangangia hali hii. Hiki ndicho kina cha masaibu yanayowakumba Wakenya wa tabaka mbalimbali. Hebu watazame Wakenya wanavyowaabudu wahubiri mataperi ambao wanasheherekea ujinga, kutokujua na upuuzi wa hali ilivyo ya mambo. Hata pale panaonekana wazi utumizi mbaya wa Injili kuwapendelea "watumishi" wa Mungu kama vile Kanyari, Nganga, Helikopta, Kiuna, na wengineo, Wakenya hawa hawa hawabanduki hawatingisiki. Wanashikilia uzi huo huo kana kwamba wamepofushwa. Tazama katika ukumbi wa kisiasa jinsi wanasiasa wanavyo watumia umaskini na kukosa kazi kwa vijana kwa kuwahusisha katika ghasia zinazowaacha manusura wakiyatibu majeraha yao baadaye bila usaidizi wa waliowachochea. Hapo ndipo tulipofika kama nchi. Na tunapojiandaa kuwachagua viongozi hapo mwaka ujao, mengi tutayaona wakati viongozi wataanza kupuriza michirizi ya chuki na uchochezi.

Add new comment

The content of this field is kept private and will not be shown publicly.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Lines and paragraphs break automatically.
  • Web page addresses and email addresses turn into links automatically.
CAPTCHA
2 + 16 =
Solve this simple math problem and enter the result. E.g. for 1+3, enter 4.
This question is for testing whether or not you are a human visitor and to prevent automated spam submissions.